Manara kumposa Wema Sepetu
TUESDAY , 24TH JAN , 2017
Mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano wa klabu ya Simba, Haji Sunday Manara amelipa mtihani mwingine Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuahidi kufanya maamuzi makubwa endapo ratiba ya ligi kuu haitabadilishwa hadi mwisho wa msimu
Haji Manara (Kushoto), Wema Sepetu (Kulia)
Maamuzi ambayo Haji ametangaza kuyafanya ni kumposa mrembo wa Tanzania (Miss Tanzania) mwaka 2006 Wema Sepetu na kumuoa endapo atakubali, lakini kama hatakubali, Haji ameahidi kutembea akiwa amevaa nguo ya ndani pekee (Boxer) kutoka nyumbani kwake hadi katika ofisi za TFF zilizoko Ilala Dar es Salaam.
"Nimalizie Kwa kuwapa mtihani mwingine TFF na bodi ya Ligi, iwapo Kama ratiba yao ya Ligi kuu na Kombe la shirikisho haitabadilishwa kuanzia sasa hadi mwisho wa msimu, ntamposa mlimbwende Wema Sepetu, na akikubali ntamuoa, akikataa ntatembea na boxer toka Nyumbani kwangu hadi TFF" Amesema Manara
Hatua hii ya Haji imekuja ikiwa ni saa chache baada ya Bodi ya Ligi kusogeza mbele mchezo kati ya Simba na Yanga uliokuwa umepangwa kufanyika Februari 18, mwaka huu na sasa utachezwa Februari 25 mwaka huu.
Hatua hiyo ya Bodi ya Ligi imekuja kama kutimiza kile ambacho Manara alikiahidi awali mwanzoni mwa msimu, ambapo alisema kuwa angetembea akiwa mtupu endapo ratiba ya ligi isingebadilishwa.
Katika tamko lake la sasa kupitia ukurasa wake wa Facebook, Manara ameeleza kusikitishwa kwake na kile alichokiita ubabaishaji katika upangaji ratiba, na kulitaja suala hilo kuwa ni moja ya sababu ya Tanzania kukwama katika soka.
"Ninajiuliza iwapo ratiba ya Ligi yetu ni muhali kuipanga,vipi kuhusu program nyingine za maendeleo? Itakuwaje kuhusu timu yetu ya taifa juu ya ndoto zetu za mchana wa jua kali? vipi kuhusiana na zile programu hewa za soka la vijana, watoto na wanawake?"
Ameendelea kusema "Hakika kwetu hayo ni sawa na bahari ya Mediterranean au bahari kuu ya hadithi za Alfu Leila uleila, hatuwezi ratiba tutaweza kwenda Afcon 2019? hatuwezi kupanga ratiba tutaweza kuwa na mipango madhubuti ya kuendeleza mchezo huu ambao yatajwa watu bilioni tatu duniani kote wanaushabikia?"
Yetu macho, je litatoke hilo. Tusubiri tuone. Hii ni sehemu ya andiko lake
Comments